Joshua 4

Ukumbusho Wa Kuvuka Mto Yordani

1 aWakati taifa lote lilipokwisha kuvuka Mto Yordani, Bwana akamwambia Yoshua, 2 b“Chagua watu kumi na wawili miongoni mwa watu, kila kabila mtu mmoja, 3nawe uwaambie wachukue mawe kumi na mawili katikati ya Mto Yordani, palepale makuhani waliposimama, wayachukue na kuyaweka mahali mtakapokaa usiku huu wa leo.”

4 cBasi Yoshua akawaita watu kumi na wawili ambao alikuwa amewachagua kutoka miongoni mwa Waisraeli, mtu mmoja kutoka kila kabila, 5 dnaye akawaambia, “Mtangulie mbele ya Sanduku la Bwana Mwenyezi Mungu wenu, mwende katikati ya Mto Yordani. Kila mmoja wenu atainua jiwe begani mwake, kufuatana na hesabu ya makabila ya Waisraeli, 6 ekuwa kama ishara katikati yenu. Siku zijazo, wakati watoto wenu watakapowauliza, ‘Ni nini maana ya mawe haya?’ 7 fwaambieni kwamba maji ya Mto Yordani yaliyokuwa yakitiririka yalitindika mbele ya Sanduku la Agano la Bwana. Wakati lilipovuka Yordani, maji ya Yordani yalitindika. Mawe haya yatakuwa kumbukumbu kwa watu wa Israeli milele.”

8 gHivyo Waisraeli wakafanya kama Yoshua alivyowaagiza. Wakachukua mawe kumi na mawili kutoka katikati ya Mto Yordani, kulingana na hesabu ya kabila za Waisraeli kama Bwana alivyomwambia Yoshua, nao wakayabeba hadi kambini mwao, mahali walipoyatua chini. 9 hYoshua akayasimamisha yale mawe kumi na mawili ambayo yalikuwa katikati ya Mto Yordani, mahali pale ambapo miguu ya makuhani waliobeba Sanduku la Agano iliposimama. Nayo yako huko mpaka leo.

10Makuhani waliobeba lile Sanduku walibakia wakiwa wamesimama katikati ya Mto Yordani mpaka kila kitu Bwana alichomwamuru Yoshua kilipokuwa kimefanywa na watu, sawasawa na vile Musa alivyokuwa amemwamuru Yoshua. Watu wakafanya haraka kuvuka, 11na mara tu watu wote walipokwisha kuvuka, Sanduku la Bwana na makuhani wakavuka watu wakiwa wanatazama. 12 iWareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakavuka mbele ya Waisraeli, wakiwa wamevaa silaha, kama Musa alivyowaamuru. 13 jKiasi cha watu 40,000 waliojiandaa kwa vita walivuka mbele za Bwana hadi nchi tambarare za Yeriko kwa ajili ya vita.

14 kSiku ile Bwana akamtukuza Yoshua mbele ya Israeli yote, nao wakamheshimu siku zote za maisha yake, kama vile walivyomheshimu Musa.

15Basi Bwana akamwambia Yoshua, 16 l“Waamuru hao makuhani wanaolibeba Sanduku la Ushuhuda, wapande kutoka ndani ya Mto Yordani.”

17Kwa hiyo Yoshua akawaamuru hao makuhani akisema, “Pandeni kutoka ndani ya Mto Yordani.”

18 mNao makuhani wakapanda kutoka ndani ya Mto Yordani wakilibeba hilo Sanduku la Agano la Bwana. Mara tu walipoiweka miguu yao penye kingo, nje ya mto, maji ya Yordani yakarudi kufurika kama ilivyokuwa kabla.

19 nSiku ya kumi ya mwezi wa kwanza watu walipanda kutoka Yordani na kupiga kambi huko Gilgali, kwenye mpaka wa mashariki ya Yeriko. 20Naye Yoshua akayasimamisha huko Gilgali yale mawe kumi na mawili ambayo walikuwa wameyachukua katikati ya Mto Yordani. 21Akawaambia Waisraeli, “Wazao wenu watakapowauliza baba zao siku zijazo wakisema, ‘Mawe haya maana yake ni nini?’ 22 oBasi waambieni, ‘Israeli ilivukia mahali pakavu katika Mto Yordani.’ 23 pKwa maana Bwana Mwenyezi Mungu wenu alikausha maji ya Yordani mbele yenu, hadi mlipomaliza kuvuka. Bwana Mwenyezi Mungu wenu alifanya haya kwa Mto Yordani sawasawa na kile alichoifanyia Bahari ya Shamu wakati alipoikausha mbele yetu hadi tulipomaliza kuvuka. 24 qAlifanya hivi ili kwamba mataifa yote ya dunia yapate kujua kuwa mkono wa Bwana ni wenye nguvu, na ili kwamba kila wakati mpate kumcha Bwana Mwenyezi Mungu wenu.”
Copyright information for SwhKC